Na. Elinipa Lupembe.
Kutokana na ongezeko la wanafunzi wanoandikishwa kuanza elimu
ya awali na darasa la kwanza katika shule za msingi za serikali na kusababisha upungufu wa madawati, Bunge la
Jamhuri ya Muungano Tanzania limetoa jumla ya madawati 400 kwa ajili ya shule za msingi
za halmshauri ya Arusha.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi wakati wa kupokea
madawati hayo Afisa Elimu Msingi halmshauri ya Arusha mwalimu Tumsifu Mushi
amesema kuwa madawati mia nne (400) tuliyopokea yamekuja wakati muafaka kwa kuwa
halmshauri ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa madawati 840 kutokana na
ongezeko la wanafunzi walioandikishwa mwaka huu 2017.
Mushi amesema kuwa mwaka 2017 halmashauri ilikisia kuandikisha
wanafunzi 9,595 badala yake waliandikishwa wanafunzi 13,030 sawa na asilimi
135.8% sawa na ongezeko la aslimia 25.8 % ukilinganisha na idadi iliyoandikishwa mwaka
jana 2016 kutoka na hali hiyo madawati haya tuliyopokea yamefanya kuwa na upungufu wa madawati 440.
Akizungumzia uwiano wa ongezeko la wanafunzi ukilinganisha na
idadi ya madarasa, Afisa Elimu huyo amesema kuwa tatizo la vyumba vya madarasa kwa
mwaka huu limepungua kwa kiasi kikubwa ingawa halijaisha kutokana na halmshauri kutoa kiasi cha
shilingi milioni 420 kutoka kwenye fidia ya deni la shamba la Lakilaki, fedha zilizotumika
kwenye ukarabati wa miundo mbinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa na vyoo.
“Kwa mwaka uliopita wa fedha 2016/17 halmashauri imetumia shilingi milioni 420 kupunguza changamoto ya vyumba vya madarasa na mpaka sasa baadhi ya
madarasa yamekamilika na mengine yako katika hatua za umaliziaji” amesema Mushi
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha Mheshimiwa Noah Lembris
ameipongeza serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa kuona umuhimu wa kutatua
changamoto ya madawati katika shule za
halmshauri ya Arusha.
Mwenyekiti Noah ameendelea kueleza kuwa licha ya halmashuri kushirikiana na wadau kutengeneza madawati zaidi
ya 5,000 lakini bado changamoto haikumalizika kutokana na idadi kubwa ya
watoto waliojitokeza mwaka huu kuandikishwa kujiunga na elimu ya awali na darasa la kwanza hali iliyotokana na serikali kutangaza utoaji wa bure.
Aidha Dk. Mahera amefafanua kuwa kwa mwaka huu wa fedha
halmashuri imejipanga kuelekeza nguvu nyingi katika ujenzi wa nyumba za walimu tatizo
ambalo linasababisha mkwamo hasa kwa shule za pembezoni pamoja na kushirikiana
na wadau kuendelea kutatua changamoto ya madawati.
“Bajeti ya mwaka huu tutajenga nyumba za walimu hasa kwenye shule zetu za pembezoni ili walimu waishi
karibu na shule jambo ambalo litaongeza tija na ufanisi katika suala zima la
ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi.” Amesisitiza Dk. Mahera.
No comments:
Write comments