Thursday, November 16, 2017

Waziri Jaffo awaonya watendaji


Dar es Salaam. Waziri wa Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jaffo ametishia kuwang’oa watendaji watakaohujumu ujenzi wa miundombinu katika Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Jaffo amesema hayo leo Alhamisi wakati akizindua jengo la ofisi na maabara itakayotumiwa na mradi huo.

Mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) utajenga barabara na mifereji kwenye jiji zima la Dar es Salaam.

Akifafanua Jaffo amesema lengo la mradi huo ni kubadilisha sura ya Manispaa ya Temeke na jiji zima la Dar es Salaam. Amesema watendaji wa manispaa wanatakiwa kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huo inakamilika.

"Sitamvumilia mtendaji yeyote atakayehujumu mradi huu, nitamng'oa bila kumwangalia usoni," amesema.

Amesema amefarijika baada ya kuona daraja la Tuangoma na barabara ya Kijichi-Tuangoma ambayo inakaribia kukamilika.

Kwa upande wake, mratibu wa mradi huo katika Manispaa ya Temeke,Edward Simon amesema Sh 265 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi barabara na mifereji. Amesema jumla ya kilometa 91 za barabara za ndani zitajengwa kwenye manispaa hiyo.

Mwananchi:

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo