Na. Sulbasia Evord.
Wananchi wa kata ya Nduruma halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru wamefurahia neema ya uendelezwaji na upanuzi wa miundombinu ya kituo cha Afya cha Nduruma ambacho kimepatiwa fedha za kukamilisha hadhi ya kituo hicho cha Afya.
Afisa Mipango halmashauri ya Arusha Anastazia Tutuba amesema kuwa serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kufanya upanuzi wa miundo mbinu ya kituo hicho ili kiwe na hadhi kufuatia vigezo vya wizara ya Afya.
Amesema kuwa fedha hizo zitatumika kujenga maabara, jengo la upasuaji, nyumba ya kuhifadhia maiti, Kliniki ya mama na mtoto, sehemu ya kuchomea taka pamoja na nyumba ya mganga.
"Licha ya kuwa kituo cha afya kilikuwepo, kituo hicho hakikuwa na hadhi ya nyota tano kutokana na upungufu wa majengo hayo yanayojengwa sasa" amesema Tutuba
Amesema kuwa serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 700 kati ya hizo milioni mia 5 zimeletwa halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na shilingi milioni 200 zimepelekwa Idara ya Uhifadhi Dawa (MSD) kwa ajili ya kununulia vifaa tiba na dawa.
Hata hivyo wananchi wa Nduruma wamefurahia ujenzi huo kwa kushiriki kutoa nguvu katika uchimbaji wa msingi wa majengo yote na wengine kukubali kufanya vibarua vya ujenzi wa majengo hayo pamoja na usimamizi wa ujenzi huo.
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi Abasia Mzava amethibitisha ushiriki wa wananchi kwenye ujenzi huo kwa kusema kuwa wananchi wamejipanga kushirikiana na serikali kuhakikisha majengo yanakamilika kwa wakati.
"Sisi wananchi wa Nduruma tumejitoa kwa hali na mali kuharakisha shughuli za ujenzi na tuko tayari kusimamia ujenzi huu mwanzo hadi mwisho ili tuweze kupata huduma ambayo inahitajika na karibu kila mtu "amesema Mzava.
Malkia Lemaya mkazi wa kijiji cha Marorani amesema kuwa majengo hayo yakikamilika itarahisisha upatikanaji rahisi wa huduma hasa kwa kina mama wajamzito ambao hulazimika kwenda kujifungulia hospitali za mjini na wakati mwingine husababisha vifo kwa kina mama na watoto.
" Ujenzi huu ni neema kwa sisi wanawake kwa hasa wajawazito wanaotakiwa kujifungua kwa operation, inabidi waende ambako ni mbali zaidi ya Kilomita 22 kwa wanaotoka Bwawani, kina mama wangine walikufa kutokana na umbali " amesema Lemaya.
Naye Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Nduruma Dkt. Dorine Moshi amesema kuwa ukamilishaji wa majengo hayo utasaidia upatikanaji wa huduma zote muhimu kwa wagonjwa wa nje na wa kulazwa.
Hata hivyo kituo kinategemea kupata ongezeko la wagonjwa kutokana na upatikanaji wa huduma zote tofauti na sasa ambapo kuna baadhi ya huduma hazipatikani na kulazimisha wagonjwa kwenda mbali kutafuta huduma hizo.
Aidha ameongeza kuwa eneo hili halina hospitali na kufanya kituo cha Afya Nduruma kuhudumia wakazi wa vijiji na vitongoji vyote vya kata ya Nduruma pamoja na kata za jirani za Mlangarini, Bwawani na Oljoro.
Hata hivyo mganga huyo ameeleza kuwa wamejipanga kutoa huduma bora kulingana na hadhi ya kituo hicho mara kitakapokamilia na kuwaondolea adha wagonjwa kutembea umbali mrefu kupata matibabu.
Afisa mtendaji kata ya Nduruma Elisha Lemungu amesema kuwa wananchi wamejitoa kwa hali na mali kutokana na umuhimu na uhitaji wa huduma zote za matibabu hasa huduma ya upasuaji na mochwari.
"Wananchi wa Nduruma wamejitoa sana kwenye ujenzi lengo ni kuhakikisha majengo yanakamilika kwa wakati na huduma ianze kupatikana haraka" amesema Elisha.
Mhandisi wa ujenzi halmashauri ya Arusha Mhandisi Bibie Manzi amesema kuwa ujenzi huo unatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu 2017 na ifikapo Januari 2018 huduma zianze kutolewa.
No comments:
Write comments