Wananchi wa kata ya Musa wametakiwa kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya ukatili kwa watoto kwa kutoa taarifa kwenye kituo maalumu cha kutolea taarifa cha Ace Africa Resources Center kilichojengwa kwa zaidi ya shilingi milioni sita kwenye kijiji cha Oloitushula kata ya Musa.
Rai hiyo imetolewa na mgeni rasmi Afisa Maboresho halmashauri ya Arusha Eline Mwanri kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa kituo hicho iliyofanyika kwenye kanisa la T.A.G katika kijiji cha Olcholovosi.
Mwanri amewataka wananchi wa Musa kutumia kituo hicho kufichua uovu unaofanywa na jamii dhidi kwa kutoa taarifa za ukatili huo pamoja na kupata miongozo ya namna ya kupata haki dhidi ya ukatili huo.
Amesema kuwa kuna tatizo kubwa la ndoa za utotoni zinazosababishwa na wazazi na walezi jambo ambalo linamsababishia mtoto wa kike kukatisha masomo hata kama ana uwezo wa kendelea na shule.
" Ukatili wa watoto unafanywa na sisi wenyewe ndani ya jamii yetu, tunapaswa kuupiga vita kwa kutoa taarifa za matukio hayo bila kuona aibu kwa jamii inayokuzunguka" amesema Mwanri
Ameongeza kuwa kituo hicho kikitumiwa vizuri kitaleta mabadiliko ya kijamii si kwa wakazi wa Musa peke yake bali kitakuwa mfano hata kwa wananchi wa maeneo mengine watakuja kujifunza hapa.
Manase Liyoki mzee wa kanisa la T.AG Olcholovosi meshukuru shirika la Ace Africa kwa kujenga kituo katika kijiji chao kwani kitasaidia wananchi kupata maarifa na kujifunza namna ya kupambana na mila na desturi kandamizi dhidi ya wanawake na watoto zinazoendelezwa katika jamii yao..
Liyoki amethibitisha kuwa kwenye jamii yao ya kimasai kumekuwa na watu wanaendeleza mila kandamizi kwa wanawake na watoto na kuongeza kuwa kupitia kituo hicho jamii itaacha mila hizo kwa kuhofia taarifa zao kutolewa kwa haraka kutokana na ukaribu wa kituo hicho.
"Wamesema kutakuwa na mtu hapo kituoni muda wote hii itasaidia jamii kuhofia kufanya uovu kwa kuhofia taarifa zitatolewa kwa kuwa hapa ni karibu na pia itaturahisishia kupata maarifa ya kujifunza juu ya mambo mengine" amesema
Mwalimu Rehema Mushi amethibitisha kuwepo na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hasa watoto wa kike ambayo watoto huchumbiwa wakiwa shuleni na umri katika mdogo pia.
Ameongeza kuwa pamoja na watoto kufanyiwa ukatili lakini jamii imekuwa inaficha uovu huo kwa kutokutoa taarifa za matukio hayo kwa hofu ya kuleta uhasama miongoni mwao na wakati mwingine sababu ya umbali wa mahali pa kutolea taarifa.
" Kupitia kituo hiki ni dhahiri jamii imesogezewa huduma za kupata maarifa yatakayowawezesha kutoa taarifa dhidi ya ukatili wa watoto jambo ambalo litapunguza vitendo hivyo viovu, watu wataogopa " amesema
Naye Ernest Lesikari Mwenyekiti wa kijiji cha Oloitushula amesema kituo hicho kitasaidia jamii yao kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa ujumla na kusaidia jifunza na kupata maekekezo ya mambo mbalimbali.
Beatrice Tengi amesema kuwa kituo hiki kitahudumia wananchi wa kata ya Musa na kata za jirani na kuwataka wananchi kufika kituoni hapo kupata taarifa mbalimbali zenye maarifa katika sekta zote ikiwemo kijamii, kiuchumi, elimu, afya, kilimo, mifugo na msuala ya kisheria.
Amesema kuwa jengeni tabia ya kufika kituoni hapo mara kwa mara ili kupata taarifa na kupata msaada wa maelekezo ya mambo ambayo mnahitaji ufafanuzi pamoja na kutoa taarifa za ukatili dhidi ya watoto na kuwahakikishia kuwa taarifa zitakazotolewa kituoni hapo zitakuwa ni za siri.
"Hiki sio kituo cha polisi ni kituo cha kupatia taarifa zenye kuwapa maarifa juu ya masuala yote yanayohitajika kwa jamii, mtapewa msaada hata wapi pa kuanzia hata kama mna migogoro ya kisheria, mmeletewa maarifa nyumbani yatumieni" amesisitiza Tengi
Agripina Bayo mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Musa amesema kuwa wao kama watoto watatumia kituo hicho kutoa taarifa pindi watakapoona kuna mtoto anafanyiwa ukatili na wazazi au mtu yoyote.
"Tunafundishwa haki, ulinzi na uasala wa watoto na tunaona ukatili unafanywa kwa watoto lakini tulikuwa hatujui pa kwenda kwa sasa tutakuja hapa kituo" amesema
Gudila Joackim mratibu kitengo cha watoto shirika la Ace Africa amesema kuwa kituo kitarahisisha jamii kupata taarifa mbalimbali muhimu kuliko kwenda kuzitafuta mjini ambapo ni mbali hivyo kupunguza gharama za kusafiri.
Ameongeza kuwa kituoni hapo jamii itapata taarifa za kilimo, ufugaji miongozo ya masuala ya kisheria na masuala ya kijamii kwa ujumla.
Hata hivyo uzinduzi huo uliambatana na mafunzo ya siku yaliyohusisha viangozi wawakilishi wa wananchi ikiwemo viongozi wa dini, siasa, serikali, mila, koo na makundi malimbali ya kijamii.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wawakilishi hao wa wananchi wa namna ya kupata maarifa na kutoa taarifa katika kituoni hapo.
Hongera wananchi wa Musa kwa kutambua fursa za maendeleo ya jamii yenu na kutoa eneo la ujenzi wa kituo hicho ambacho kitaleta mabadiliko kwa jamii ya wanamusa na Taifa kwa ujumla.
PICHA ZA MATUKIO YA UFUNGUZI WA KITUO CHA ACE AFRICA RESOURCES.
No comments:
Write comments