Utekelezaji wa mradi wa maji wa vijiji vitano halmashauri ya Arusha maarufu kama mradi wa maji wa WaterAid umeendelea kupata baraka za wananchi katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo.
Baraka hizo zimetolewa na wajumbe wa serikalo ya kijiji cha Lengijave walipokutana na kamati ya usimamizi wa mradi huo halmashauri Arusha kwenye ofisi za kata ya Olkokola wakati wa kikao cha utekelezaji wa mradi huo.
Timu hiyo ya usimamizi wa mradi walipata fursa ya kuelezea mradi huo wa maji kuwa utakuwa wa mfano kutokana na mkakati wa utekelezaji wa mradi unaoendana na ushirikishwaji wa jamii husika, utunzaji wa mazingira ili kupata maji safi na salama, pamoja na ulipiaji wa huduma ya maji kwa kutumia teknolojia ya kulipa kabla ya kutumia maji ya eWaterpay.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Arusha ndugu Angela Mvaa amewaelezea wajumbe wa serikali ya kijiji cha Lengijave kuwa licha ya kuwa mradi huo utagharamiwa na wafadhili kwa asilimia mia moja lakini pia jamii ina wajibu wa kushiriki katika mradi huo kwa kuukubali na kutambua mradi huo ni wao na kutambua thamani ya rasilimali maji sambamba na kuitunza.
Ameongeza kuwa kutokana na changamoto ya maji inayoathiri shughuli nyingine za kiuchumi jamii pia inatakiwa kuona umuhimu wa mradi kwa kukubali miundo mbinu ya maji kupita katika maeneo yao pamoja na kulipia gharama za maji ili huduma hiyo iweze kuwa endelevu.
Aidha Afisa Ardhi Mteule ndugu Rehema Jato ameeleza kuwa mradi huo wa maji unatumia fedha zilizotolewa na wafadhili na hawakutoa fedha kwa ajili ya fidia ya ardhi hivyo wananchi wanatakiwa kushiriki kwa kukubali miundo mbinu ya maji kupita katika maeneo yao bila kufidiwa gharama yoyote licha ya kuwa ni takwa la kisheria kulipa fidia.
"Wenzetu wamejitolea kutusaidia kutokana na shida ya maji inayotukabili na kila mtu hapa ni dhahidi wa adha hii ya maji kwa hiyo na sisi tunatakiwa kuwaunga mkono wenzetu kwa kujitolea maeneo yetu kwa kuruhusu kupitisha mabomba ya maji kwenye mepaeneo yetu.
Hata hivyo Jato ameongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo wataalamu watajitahidi kupitisha bomba kwenye maeneo ya pembezoni mwa barabara lakini pale inapobidi kukata mgomba wa mtu, ni vema kukubali kujitolea kufanya hivyo.
Naye Afisa Usafishaji na Mazingira amesisitiza kuwa mradi huu utaambatana na utunzaji wa mazingira ya vyanzo vya maji pamoja na utunzaji wa maji na miundo mbinu ya maji hayo kwa ujumla wake.
Aidha amewaomba wananchi hao kuacha kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya mita sitini kwenye vyanzo vya maji na kuwataka viongozi hao kuelimisha jamii yao kuacha tabia hiyo.
Ameongeza kuwa kuna athari kubwa kwa afya ya binadamu zinazotokana binadamu kunywa maji yaliyochafuliwa na vinyesi vya binadamu na wanyama, mifuko ya plastiki na pampasi za watoto.
" Yatupasa kufahammu hili mtu akinywa maji yaliyochanganyika na gramu moja ya mavi anakunywa bakteria milioni kumi pamoja protozoa elfu moja hali ambayo inasababisha magonjwa yasiyoisha kwenye jamii zetu" amesema
Hata hivyo viongozi hao wa serikali ya kijiji wamesema kuwa wako tayari kushiki kwa hali na mali kwenye hatua zote za utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa kiu yao kubwa na kupata maji safi na salama katika kijiji chao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Lengijave ambaye pia ni diwani wa kata ya Olkokola mheshimiwa Kalanga Laiza amethibitisha kuwa wananchi wa Lengijave hawana tatizo la maendeleo kwenye kijiji na kuwa wako tayari kushiriki hatua zote kwani ni tabia yao.
" Utunzaji wa mazingira kwenye kata yangu ni agenda ya kudumu tulianza rasmi mwaka 2002 tulipanda miti yote unayoiona na hakuna ng'ombe anayeingia shamba, hivyo niwatoe wasiwasi wananchi hawa wako tayari kushiriki kwenye mradi huo wa maji" amesema Kalanga
Ameongeza kuwa wananchi wako tayari kulipia huduma ya maji na kusisitiza kuwa upangaji wa gharama hizo za maji zizingatie hali halisi ya kiuchumi ya maisha ya wananchi wa maeneo ya vijijini kwa kuwa wengi hawana uwezo mkubwa wa kifedha.
Naye mwanzilishi wa mradi huo Mratibu wa shirika lisilo la serikali la Tumaini Jipya Louise Richardson amesema kuwa hamu yake kubwa ni kuona wananchi Lengijave wanapata maji safi na salama na kuwataka wananchi kushiriki kwenye mradi huo kama wanavyoelekezwa na wataalam.
"Tukipata maji safi na salama tutaepuka magonjwa na familia zitakuwa na afya njema na familia zitakuwa salama" amesema Louise.
Mradi huo wa maji unafadhiliwa na shirika la Maendeleo nchini Uingereza (DFID) na kutekelezwa na shirika la WaterAid utakaogharimu takribani shilingi Bilioni 4.5 n kuhudumia jumla ya watu elfu hamsini wa vijiji vya Lengijave kata ya Olkokola na Okokola kata ya Lemanyata na vitongoji vya Seuri na Ekenywa kata ya Olturumet na kitongoji cha Ngaramtoni kata ya Olmoton.
Picha za matukio za kikao.
No comments:
Write comments