Ngara.Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Agustino Ollomi amewataja majina wanafunzi ambao wamefariki dunia kutokana na bomu la kutupwa kwa mkono katika shule ya msingi Kihinga wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
Kamanda Ollomi amesema kwamba wanafunzi hao ni Juliana Tarasisi (13) Evart Theonas (12) Edson Bigilimana (12), Miburo Gabriel (12), na Tumsifu Ruvugo (8).
Pia Kamanda huyo amesema mtoto wa sita aliyedhani amefariki alibainika kuwa bado yuko hai na yuko mahututi kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).
Amesema mwalimu wa darasa, Policalipo Clemency aliyekuwa darasani wakati wa tukio ni miongoni mwa waliojeruhiwa na kulazwa hospitali.
Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu Clemency amesema wakati bomu linaipuka, alikuwa akiandika mtihani wa kusoma ubaoni na kila mwanafunzi alikuwa akiingia na kusoma ili kumwekea alama kwa ajili ya mitihani ya kufunga mwaka.
“Ghafla nilisikia kishindo kikubwa na kuona baadhi ya wanafunzi wakianguka, walipoteza fahamu na wengine kutokwa damu,” amesema Clemency
Mmoja wa wazazi aliyepoteza mtoto katika tukio hilo, Bigimana Kaloli amesema baada ya kusikia kishindo alikimbilia shuleni na kusikia mtoto wake anayeitwa Edson akiwa tayari amefariki na kusema jambo hilo limeipa familia yake simanzi kubwa.
Mwananchi:
No comments:
Write comments