Halmashauri ya Arusha imejipanga kutoa mafunzo mafupi kuhusu matumizi sahihi ya fedha za Mpango wa Kunusuru kaya Masikini zinazotolewa na serikali kupitia mradi wa TASAF awamu ya III kwa wanufaika wa Mpango huo kila wakati wa zoezi la malipo ya wanufaika hao linapofanyika.
Uamuzi huo umefikiwa kutokana na baadhi ya waniufaika wa mpango huo kuonekana kutumia fedha hizo kwenye ulevi na mambo mengine yasiyofaa kinyume na malengo ya mradi huo na kusababisha baadhi yao kupunguziwa malipo kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya fedha hizo na wengine kusababisha migogoro kwenye familia.
Akizungumza wakati wa kugawa fedha hizo kwa kaya 189 za kijiji cha Ilkirevi kata ya Olturoto kwenye Ofisi za Kijiji hicho mwezeshaji ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Mwandeti ndugu Paulina Masoka amesema kuwa tumejipanga kutumia muda mfupi kabla ya kugawa fedha kwa lengo la kuwakumbusha wanufaika wa mpango kutumia fedha hizo kutokana na masharti ya TASAF.
Masoka amefafanua kuwa kuna baadhi ya wanufaika wanashindwa kutekeleza masharti ya matumizi ya fedha hizo ikiwemo kuwahudumia watoto wanaosoma, kuwapeleka watoto kliniki pamoja na kuhudumia familia na badala yake wanatumia fedha hizo kwenye ulevi.
"Inatulazimu kuwakumbusha wasimamizi hawa wa kaya kutumia fedha hizo kutunza familia kwa kuwa imeonekana baadhi yao wakipata hela wanaishia kwenye pombe na kusababisha familia kuendelea kuteseka" amesema Masoka
Masoka ameongeza kuwa mafunzo tutakayoendelea kuyatoa pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa wanufaika hao yatasaidia kutatua changamoto hiyo kuliko kukaa kimya kuwaacha bila kuwakumbusha.
Hata hivyo wasimamizi wa kaya hizo waliofika kupokea ruzuku hizo wanajivunia kutumia kiadi cha shilingi elfu kumi kukata kitambulisho cha Bima ya Afya ya Jamii jambo ambalo limewarahisishia upatikanaji wa matibabu pindi wanapougua.
Wameongeza kuwa waliposhawishiwa kujiunga na mfuko huo walidhani ni utapeli lakini wamethibitisha kutambua umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya ya Jamii kwani imeondoa makali ya gharama za matibabu.
Nembris Paulo (60) mkazi wa kijiji cha Ilkirevi amethibitisha kufaidika kwa matibabu baada ya kutumia fedha aliyoipata TASAF kujiunga na Bima ya Afya ya Jamii kutokana na ugonjwa wa pumu ambao una,sumbua na unahitaji matibabu ya mara kwa mara na wakati mwingine alishindwa kutibiwa kwa kukosa fedha lakini sasa amekuwa akitibiwa bila kulipia.
"Tangu nimekata Bima nimepona kifua kwa kuwa nimepata matibabu mazuri kwa utaratibu, zamani nilikuwa nikiandikiwa dawa nanunua nusu nusu sababu sikua na pesa baada ya kupeleka Bima nimetibiwa vizuri na nimepona sisumbuliwi mara kwa mara kama zamani "amesthibitisha Nembris.
Naye mratibu wa TASAF halmashauri ya Arusha Jabir Ali amesema kuwa kwa sasa wanalipa awamu ya 14 tangu mradi huo kuanza na awamu hii wamelipa jumla ya shilingi milioni 290.9 kwa kaya 9121 kwenye vijiji 45 ndani ya halmashauri ya Arusha.
Jabir amesema kuwa licha ya kuwa fedha hizo zinawasaidi wananchi hao lakini bado kuna changamoto ya baadhi ya wanakaya kushindwa kutimiza masharti jambo ambalo linasababisha mwana kaya kukatwa kiasi cha fedha.
Hata hivyo Jabir amesema kuwa kupitia maafisa wa halmashauri wanaokwenda kusimamia zoezi la ulipaji wa fedha kuhakikisha wanatoa mafunzo ya kuwakumbusha wanufaika hao kutumia fedha hizo kulingana na masharti ya TASAF.
Aidha amewataka wananchi wote wanaonufaika na Mpango kutumia fedha hizo vizuri pamoja na kutunza vitambulisho vyao vya TASAF na kuepuka kutuma mtu wa kumchukulia fedha jambo ambalo haliruhusiwi na linasababisha fedha kurudishwa.
Picha za matukio wakati wa zoezi la ugawaji wa fedha kijiji cha Ilkirevi kata ya Olturoto.
No comments:
Write comments