Ule usemi usemao penye wengi hapaharibiki neno umejidhihirisha kwa wakazi wa vitongoji vya Tarakwa na Saitabau kata ya Tarakwa halmashauri ya Arusha baada ya kufanya Mkutano wa pamoja na viongozi wao kwa lengo la kujadili migogoro ya kisiasa baina ya viongozi iliyokuwa ikikwamisha maendeleo katika maeneo yao.
Mkutano huo ulioitishwa na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera baada ya wananchi hao kuwa na malalamiko ya muda mrefu yaliyosababisha wananchi kuacha kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.
Licha ya Mkutano huo kuwa na maswali, maoni, kero na malumbano ya hapa na pale hatimaye ulimalizika ukiwa na matokeo chanya kwa makubaliano ya kuondoa tofauti zao kwa kuachana na mambo yaliyopita kwani yamechelewesha maendeleo yao na kuamua kuanza upya kama familia moja ya wanatarakwa ndipo usemi wa penye wengi hapaaribiki neno ulipojidhihirisha.
Awali wananchi hao walipata fursa ya kutoa kero zao na walilalamikia kunyang'anywa mradi wao wa maji na Mamlaka ya Maji Ngaramtoni NGAUWASA mradi waliojengewa na wafadhili na ulikuwa ukisimamiwa na kamati ya maji walioichagua.
Zaidi wananchi hao wa Tarakwa walionyesha kutoridhika kata yao kuingizwa kwenye Mamlaka ya Mji mdogo Ngaramtoni pamoja na vitongoji vyao kukosa umeme, maji yasiyo aminika, miundo mbinu mibivu ya barabara, kutokuwa na zahanati pamoja na shule ya sekondari.
Hata hivyo Mkurugenzi Mahera aliongoza jopo la wataalam wa Halmashauri kuelezea na kuwaelemisha kata yao kuingia Mamlaka ya Mji mdogo na faida za kuwa dani ya mamlaka ambayo kibwa zaidi ni kupandisha hadhi ya maeneo yao kutoka vijiji kuwa mji ili kuharakisha maendeleo pamoja na kasi ya upatikanaji wa huduma za jamii.
Aidha Dkt. Mahera amefafanua kuwa eneo linapokuwa ndani ya mamlaka ya Mji, miradi ya maji inalazimika kusimamimwa na Mamlaka ya Maji ya eneo husika hivyo miradi ya maji ya eneo hili itasimamiwa na mamlaka ya maji NGAUWASA na kuua kamati za maji.
"Ni vema makafahamu kuwa ili huduma ya maji ya maji iwe endelevu lazima ilipiwe kulingana na eneo husika hakutakuwa na huduma ya maji itakayotolewa bure wananchi mnapaswa kujipanga kwa hilo" ameweka wazi Mkurugenzi huyo
Hata hivyo wananchi wa Tarakwa baada ya ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa hoja walizoziwasilisha walifikia muafaka wa kuachana na migogoro iliyokuwepo na kuamua kuanza upya kujipanga kwa ajili ya maendeleo ya kata yao.
Wananchi hao walikubaliana kuanza upanuzu wa barabara inawaunganisha na barabara kuu iendayo Namanga ambayo tayari mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo alitoa lita mia moja za mafuta ya mitambo na halmashauri kuongeza lita 100 pamoja na kutoa mitambo, walikubaliana pia kujipanga kutafuta eneo la kujenga shule ya Sekondari na Zahanati.
Shime wananchi wa TARAKWA wekeni tofauti zenu pembeni jipangeni kwa ajili ya maendeleo yenu na taifa.
Picha za matukio ya mkutano huo
No comments:
Write comments