Wanawake wajawazito kata ya Ilkiding'a wametakiwa kuacha tabia kujifungulia kwa wakunga wa jadi badala yake kutumia Zahanati zilizopo katika maeneo yao kupata huduma zote za afya ya mama na mtoto kwa kuwa zipo kwaajili yao
Hayo yamesemwa na mwezeshaji wa shirika la EngenderHealth bi. Delfine Msele wakati wa mafunzo yaliyohusu huduma ya uzazi na afya ya mama na mtoto yaliyowakutanisha viongozi ya jamii wa vijiji vitatu vya kata ya Ilkiding'a na wahudumu wa afya wa halmashauri ya Arusha yaliyofanyika kwenye Zahanati ya Kiyoga kata ya Ilkiding'a.
Msele amesema kuwa ni vyema jamii ikafahamu umuhimu wa kina mama wajawazito kujifungulia kwenye kituo cha afya pamoja na wanaume kuambatana na wake zao kliniki wakati wote wa kipindi cha ujauzito.
Msele amesema kuwa ripoti ya mwaka 2015 inaonyesha wanawake wanaofika kituoni kujifungua ni 146 kati ya wanawake 416 waliojifungua katika kata ya Ilkiding'a sawa na asilimia 38% jambo ambalo linaashiria hatari kubwa kwa kinamama na watoto wanaozaliwa pamoja na wakunga wanaowazalisha.
Ameendelea kufafanua kuwa kuna hatari kubwa ya kutokea vifo kwa mama na mtoto wanaozalishwa nyumbani kwa wakunga wa jadi kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua.
Aidha amesema kuwa licha ya vifo kutokea pia kuna uwezekano mkubwa wa maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na hata mkunga kupata maambukizi.
" Kama viongozi wa jamii tunatakiwa kupiga vita kina mama wajawazito kwenda kujifungua kwenye vituo vya afya kwa kuwa serikali imeleta wataalamu wa afya kwa ajili ya usalama wa afya ya mama na mtoto"amesema Msele.
Kaimu Muuguzi Mkuu Halmashauri ya Arusha Agusta Komba amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuitaka jamii kuzitambua huduma zinazotolewa kwenye vituo vyao vya afya pamoja na kuzimiliki huduma hizo kama mali yao na si mali ya serikali kwa kuwa serikali ni msimamizi wa huduma hizo.
"Zahanati hii ni mali yenu wanajamii serikali ni msimamizi tuu hivyo mnatakiwa kuzifahamu huduma zote zinazotolewa na kuzimiliki kwa kuzitumia kwa kuwa ni zenu, mnatakiwa kufahamu changamoto na mafanikio ya kituo chenu na si mtu mwingine" amesisitiza Komba
Hata hivyo Komba amesema kuwa wameandaa mpango mkakati wa kutoa mafunzo hayo shirikishi yenye kushirikisha jamii kupitia viongozi wa mila, dini, kisiasa, kiserikali na wahudumu wa afya ambayo yanahusisha kutembelea zahanati na vituo vya Afya kujionea haduma za uzazi zinavyotolewa kuanzia mama mjamzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua ambayo yatafanyika kwenye vituo vyote vya afya hasa kwenye maeneo ambayo yanachangamoto ya wajawazito kujifungulia nyumbani.
Nao viongozi wawakilishi wa jamii kupitia makundi mbalimbali waliohudhuria mafunzo hayo wamekubaliana kwa pamoja kukaa na wananchi kuona namna ya kuchanga fedha kwa ajili ya kimarisha na kuboresha miundombinu ya Zahanati hiyo.
Mafunzo hayo yanayojulikana kama 'Walking Through' yanajumuisha mafunzo na matembezi ya kutembelea na kukagua Zahanati hiyo ya Kiyoga kujionea namna huduma za uzazi zinavyotolewa kwa lengo la kujifunza na kufahamu mahitaji ya Zahanati hiyo ambayo jamii inapaswa kuchangia.
Picha za matukio ya shughuli hiyo.


No comments:
Write comments