Uko uwezekano mkubwa wa Baraza la Mawaziri kutikisika baada ya mawaziri kadhaa waliopo na wale walioondolewa kutajwa mara kadhaa katika taarifa za kamati maalumu za bunge kuchunguza biashara ya Tanzanite na almasi.
Aidha taarifa zote mbili ziliwataja kwa majina watu kadhaa wakiwemo mawaziri waliopo katika baraza la sasa kwa kujihusisha moja kwa moja katika maamuzi yaliyopindisha sheria na kukiuka utaratibu.
Kamati zote mbili zilizungumzia kwa undani hasara kubwa zilizopatikana kutokana na ushauri mbovu na usimamizi dhaifu katika mkataba wa kuuza hisa katika kampuni ya almasi mwaka 1994 ambao hazikusaidiwa na pia ubia wa Stamico na Tanzanite One Mining Limited (TML) ambapo unaelezwa uliharakishwa na Waziri George Simbachawene.
Pia, Stamico ilionekana kutofuatilia mikataba yote huku baadhi ya watendaji wa sasa wakibariki ubia huo na kusema kwamba ulikuwa ni msaada mkubwa kwa Stamico.
Pia imeelezwa kuwa hakuna taarifa sahihi kuhusu uzalishaji na uuzaji wa tanzanite ingawa duniani mauzo ni dola trilioni 8.582 katika miaka 12 iliyopita huku takwimu za Tanzania zikionesha kwamba mauzo ni bilioni 454 tu kwa kipindi hicho.
Imeelezwa kuwa ni asilimia 20 ya uuzaji wa tanzanite unajulikana nchini lakini 80 husafirishwa kwa njia ya panya.
Aidha, katika uchunguzi uliofanywa na kamati hizo ulibaini kwamba baraka zilizotolewa kwa Sky zilikuwa kinyume kwani kampuni hiyo haina usajili nchini wala haitambuliki brela.
Waziri mkuu anena
Taarifa za kamati maalumu za Bunge zilikabidhiwa jana kwa Spika wa Bunge kabla ya yeye naye kukabidhi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye naye alisema kwamba anazifikisha kwa Rais John Magufuli leo saa nne na nusu kwa hatua zaidi.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hizo Waziri Mkuu alishukuru kazi njema iliyofanywa na kamati hizo na kuahidi kwamba yote yaliyozungumzwa yatafanyiwa kazi katika kipindi kifupi kijacho.
Alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano kamwe haitamwacha mtu ambaye anakiuka katiba kwa kuacha kulinda maliasili za taifa huku akikariri Ibara ya 27 ya katiba ya mwaka 1977 kama muhuri tosha kwa kila Mtanzania.
“27 (1) kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na Wananchi na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.
“(2) Watu wote watatakiwa na Sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya nchi na pamoja vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu na kuendesha uchumi wa Taifa na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndiyo waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.” Alisema serikali itaendelea na jitihada za kuleta mageuzi katika madini ili rasilimali hizo zinufaishe Watanzania wote.
Pamoja na hatua za haraka kuchukuliwa alisema kwamba sheria ya madini, petrol, kodi ya mapato zitafanyiwa marekebisho ili kuimarisha mifumo ya kusimamia madini na rasilimali nyingine za taifa.
Alisema ni lazima kuchukua hatua kali kwa wahusika wote na kuwataka Watanzania kwenda pamoja katika vita hiyo iliyoanzishwa na Rais John Magufuli.
Mmoja wa mawaziri aliyetajwa mara kadhaa kwa ni George Simbachawene ambaye kwa sasa ndiye Waziri katika Ofisi ya Rais Tamisemi ambaye alishawahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Waziri huyo alitajwa kuhusiana na biashara ya Tanzanite ambaye aliridhia mabadiliko katika mauzo ya kampuni uchimbaji Tanzanite na utoaji wa leseni kinyume na utaratibu.
Aidha Naibu Waziri Edwin Ngonyani naye ametajwa hasa kuhusiana na kadhia ya kuzuia serikali kununua mgodi wa almasi kwa dola milioni 10 na kuikosesha serikali zaidi ya dola milioni 300, fedha ambazo zilienda kwa kampuni iliyonunua hisa.
Aidha kamati hiyo ilihoji namna ambavyo walioshiriki kukataa serikali kununua mgodi huo wa almasi walivyopata bahati ya kuchaguliwa katika bodi ya waliouziwa hisa.
Aidha taarifa zote mbili zimehoji tabia iliyooneshwa na watendaji mbalimbali wa kutochukua maamuzi na kuishia kusema kwenye mahojiano kwamba waliona ni upuuzi na wizi mtupu kuendelea kufuatia masuala ya ndani yanayogusa mikataba na uendeshaji.
Kitendo cha Eliakim Maswi kusema kwamba alipatwa na hasira baada ya kutoka katika mgodi huo wa almasi na kujionea madudu na kuapa kutokanyaga tena kulielezwa na kamati hizo kuwa moja ya sababu ya watendaji kuacha mambo yakiharibika.
Aidha aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo alitajwa kupindisha mambo kadhaa na kufanya maamuzi bila kushirikisha bodi zinazotakiwa na hivyo kusababisha hasara kubwa.
Watu wengine waliotajwa katika taarifa zote mbili ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu Nishati na Madini, Eliakim Maswi, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngereja, mwanasheria wa zamani George Werema
Pamoja na kuelezwa kuwa serikali imepata hasara ya matrilioni kutokana na mikataba mibovu, na kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa watendaji na watumishi wa umma, pia kuna makampuni yanachimba almasi na kuuza bila kufuata utaratibu. Makampuni yaliyotajwa ni matatu yakiwemo Caspian na Midwest.
Mikataba iliyozungumzwa na kuambiwa ina walakini mkubwa ni pamoja na umiliki wa Mwadui na mkataba wa Stamico na Tanzanite One Mining Limited, mkataba ambao ulizaa migogoro ya madeni makubwa kwa upande wa Stamico na kuiacha ikiwa hoi na deni la dola milioni 4. Spika Job Ndugai alisema kutojipanga kwa watu wa Stamico kumefanya kampuni hiyo kuingia katika hasara kubwa huku sera zikiwa hazifuatwi wala sheria.
Ukiukaji wa kitaasisi Kuwepo kwa ukiukaji wa taratibu na kanuni za kitaasisi na kiutendaji pia zilielezwa kutoa mwanya wa kampuni ndani ya mgodi wa almasi wa Mwadui kufanya wanachotaka, huku takwimu za uzalishaji na mauzo za TMA na Wizara ya Nishati na madini zikipishana.
Aidha hata akiba ya almasi iliyopo imeelezwa kuwa si ya uhakika kutokana na serikali kutojua akiba hiyo ikitegemea taarifa zaidi kutoka kampuni ya Mwadui ambayo kwa muda sasa wanasema wametengeneza hasara na hivyo kutolipa kodi Kampuni ya Mwadui imekuwa hailipi kodi kuanzia mwaka 2007 hadi 2017 kwa kisingizio kwamba wamepata hasara, hali ambayo haiendi sambamba na uwekezaji mkubwa unaoendelea hadi mwaka 2023.
Kamati ilisema usahihi wa takwimu ndiyo msingi wa kufanya biashara, lakini wakati Williams wanazo takwimu na wanazitumia taasisi za serikali na serikali yenyewe takwimu zake zinagongana huku nyingine zikionekana ‘kupikwa’ kutokana na kuwiana wakati sheria na muda ni tofauti.
Aidha takwimu hizo zimekuwa haziendi kwenye uhalisia wa kipindi cha sheria na maagizo ya kisheria yaliyopo. Tofauti kubwa inayooneshwa katika takwimu za wizara na taasisi ya TMAA za uzalishaji na pia na TRA katika mauzo.
Katika maelezo yote kamati ya Zungu ilihoji fedha kiasi cha Sh bilioni 7 na milioni 700 ambazo hazijaingia serikalini wakati inajulikana pia kwamba almasi ya Tanzania ndiyo ghali lakini inauzwa kwa bei ya kutupwa katika soko.
Aidha kumezuka sintofahamu ya akaunti ya mrabaha kutoka kampuni ya almasi ambapo inadaiwa ilifunguliwa akaunti NMB ambayo hata katibu mkuu alikuwa haifahamu, huku suluhu ya kibenki ikiwa haitumiki kuoanisha takwimu za mapato.
“Mrabaha wa bilioni 100 ulivyopokelewa na kuhamishwa katika kaunti haueleweki,” inasema taarifa hiyo ikionesha kuwapo na ubadhirifu mkubwa wa fedha kutokana na kukosekana kwa uwajibikaji na ufuatiliaji.
Pamoja na mikataba mibovu kuna shida ya uangalizi wa almasi yenyewe ambapo hata watendaji wa serikali (walinzi) hawapo katika maeneo nyeti kama katika x ray na chumba maalumu cha hifadhi; huku Williamson wakiuweka mgodi wa almasi rehani kufuatia madeni ambayo kiukweli hayajapitishwa wala kuhakikiwa na Benki Kuu kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa taarifa za takwimu Tanzania kwa namna ilivyo sasa imeweka rehani almasi yenye thamani ya trilioni 80 na milioni 800. Ilielezwa kuwa kuna deni la dola milioni 238 ambalo halijahakikiwa na benki kuu wala halijulikani limefikia hapo kwa namna gani ni muhimu kuangaliwa.
Ushauri wa kamati Kwa upande wa kamati ya Dk Bitego iliyochunguza tanzanite kuna haja ya kuwawajibisha wote waliohusika kuliingiza taifa hili katika mikataba mibovu isiyokuwa na tija na kuleta hasara.
Aidha wametaka watumishi waliotajwa wote kuhojiwa tumefikaje hapa huku wakitaka kutungwa sheria maalumu kuhusiana na madini hayo yanayopatikana Mererani pekee duniani kote.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli anapokea taarifa hiyo ya uchunguzi wa madini kutoka kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, Ikulu Dar es Salaam leo.
No comments:
Write comments