Wiki moja baada ya kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu Serikali imeunda kikosi kazi kushughulikia uvunjifu wa amani nchini.
Kikosi hicho kinachoshirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama pia kinashughulika na kukusanya silaha za kivita ambazo zimekuwa zikitumika.
Lissu alijeruhiwa kwa risasi Alhamisi Septemba 7 nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu jijini Nairobi, Kenya.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amesema hayo bungeni leo Alhamisi akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuf Salim Hussein.
Mbunge huyo amesema hana wasiwasi na uimara, uwezo na weledi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kusimamia majukumu yake ndiyo maana nje ya mipaka ya nchi ni salama lakini ana wasi wasi kuhusiana na hali ya usalama nchini.
“Lakini ndani ya nchi yetu hali si salama na mifano miwili ya juzi ya mbunge (Lissu) na Meja Jenerali mstaafu Vincent Mritaba inadhihirisha kwamba ndani ya nchi yetu tuna matatizo, je ni kwa nini Jeshi la Wananchi lisishiriki kikamilifu kuondosha matumizi ya silaha na mauaji ya raia wasio na hatia ndani ya nchi yetu?” alihoji mbunge huyo.
Amesema anavyoona yeye silaha za kivita zinamilikiwa na JWTZ na matumizi yake yanatakiwa yawe ya chombo hicho.
Mbunge huyo alihoji ni kwa nini wasitumike askari maalumu kuhakikisha silaha za kivita zinazotumika vibaya kuua raia zinakamatwa.
Waziri Mwinyi akijibu swali hilo amesema ni dhahiri kwamba kazi ya JWTZ ni ulinzi wa mipaka lakini pale linapohitajika au kuombwa kusaidia mamlaka zingine za kiraia au vyombo vingine vya ulinzi na usalama huwa tayari kufanya hivyo.
“Tunavyozungumza ni kwamba, mamlaka hizo ambazo ni vyombo vingine vya
ulinzi na usalama vikihitaji msaada wa jeshi mara zote tunakuwa tayari kutoa msaada huo, kwa hali ilivyo sasa imeundwa
task force (kikosi kazi) inayojumuisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama ili kulifanyia kazi tatizo hili la uvunjivu wa amani ndani ya nchi,” amesema.
Amesema hana shaka na kazi hiyo imeanza, hivyo kuwahakikishia wananchi kuwa jukumu hilo litafanywa vyema ili hali ya usalama iwepo ndani ya nchi.
Dk Mwinyi amesema ni kweli silaha za kivita zinadhibitiwa na JWTZ na kwa kutumia kikosi kazi hicho, watakusanya silaha hizo
kutoka kwa raia au watu wengine wote ambao wanamiliki silaha hizo ambazo kwa kawaida, utaratibu na kisheria hawapaswi kuwa nazo.
Amesema zitakapopatikana silaha hizo zitarudishwa katika mamlaka zinazohusika.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Mkoani (CUF), Twahir Awesu Mohamed alihoji Serikali imejipangaje kuimarisha amani nchini.
Waziri Mwinyi amesema JWTZ imejipanga kikamilifu kuhakikisha mipaka ya nchi inalindwa muda wote dhidi ya adui yeyote atakayejitokeza kuivamia.
“Jeshi letu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, limeimarisha ulinzi katika maeneo ya mipaka yenye wakimbizi ,” amesema.
Amesema hatua hiyo imesaidia kuzuia na kukabiliana na vitendo vya kihalifu vinavyowezwa kusababishwa na wakimbizi katika mipaka na katika makambi.
No comments:
Write comments