Tanga. Wakuu wa mikoa iliyopo Kanda ya Kaskazini wamejiwekea mkakati endelevu wa kukagua mafuta kwenye vituo vilivyopo katika maeneo yao ikiwa ni kufanyia kazi agizo la Rais John Magufuli aliyetaka mafuta yanayoingia nchini kupitia Bandari ya Tanga yauzwe kwa bei ya chini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela amesema kuwa yeye na wakuu wa mikoa wenzake, Joel Bendera wa Manyara, Anna Mghwira wa Kilimanjaro na Mrisho Gambo wa Arusha wameweka mkakati wa pamoja wa kuendesha ukaguzi wa kila kituo cha mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kujua kama yanauzwa kwa bei inayolingana na bei iliyokokotolewa.
“Hili la mafuta tayari mimi na mwezangu, Bendera, Mghwira na Gambo tumeshaanza kufanyia kazi tangu siku ya Alhamisi ukaguzi unaendeshwa na tutahakikisha tunapita vituoni kujiridhisha kama wauzaji wa mafuta wanayauza kwa bei ya Tanga au ya kutoka Dar es Salaam,” alisema
Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Manyara na Arusha kufanya ukaguzi kwenye vituo vya mafuta kuhakikisha yanayotolewa Tanga yanauzwa kwa bei ya chini kuliko ya Dar es salaam wakati akiweka jiwe la msingi la upanuzi wa maghala ya Kampuni ya GBP Jijini Tanga.
Aidha Rais Magufuli alisema ameamua kutoa agizo hilo ili uwekezaji uliofanywa na kampuni ya GBP jijini Tanga wa maghala ya kupokea mafuta kutoka nchi za Uarabuni yaweze kuuzwa kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini na hivyo kuondoa msongamano katika Bandari ya Dar es salaam.
No comments:
Write comments