RAIS John Magufuli amesema amedhamiria kwa dhati kuleta maendeleo nchini, kupitia uwekezaji na uzalishaji mali katika uchumi wa viwanda; na pia amedhamiria kuufungua kiuchumi Mkoa wa Tanga.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanafanya kwa bidii shughuli za uzalishaji mali ikiwemo mboga, vyakula na matunda ili kukidhi mahitaji ya soko, litakalotokana na mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Chongoleani jijini Tanga ambako kesho ataweka jiwe la msingi na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti akiwa katika miji ya Mkata, Komkonga, Kabuku, Hale, Muheza na Mkanyageni katika wilaya za Handeni, Korogwe na Muheza, alipozungumza na wananchi wakati alipowasili mkoani Tanga kuanza ziara yake ya kikazi.
Dk Magufuli alisema pamoja na ziara hiyo, ataweka jiwe la uzinduzi wa mradi wa bomba la mafuta Chongoleani jijini Tanga. Alisema mradi huo utafungua fursa za kiuchumi mkoani huko na kuwataka wananchi kuchangamkia. Tanga inazaliwa upya “Mradi huu wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga utatoa ajira zaidi ya 45,000 za kudumu pamoja na vibarua, lakini pia kundi jingine la wananchi wa Mkoa wa Tanga litapata ajira mbadala kupitia biashara mbalimbali za kuuza vyakula, kujenga nyumba za kupangisha,” alisema Dk Magufuli.
Aliongeza, “Nataka niifufue upya Tanga hii ya watani wangu ili tulete maendeleo. Tanga inazaliwa upya, Tanga sasa inafunguka. Inafunguka kupitia uwekezaji bomba la mafuta hivyo nawataka sasa tujifunze kufanya kazi kwa bidii kwa sababu hakuna vitu vya bure lazima tufanye kazi ili kuzalisha mahitaji ya chakula na vitu mbalimbali vitakavyotumiwa na wafanyakazi kwenye mradi huo.”
Alisema Tanga ilikuwa ikisifika kwa uchumi wa viwanda katika miaka ya nyuma, lakini katika miaka ya karibuni uchumi wake umedorora, lakini kuanzishwa kwa bomba la mafuta na miradi mingine ikiwamo ya kiwanda kikubwa cha saruji kinachoanzishwa, kitaufanya mkoa huo kuinuka tena kiuchumi. Aagiza uchunguzi Handeni Aidha, Rais Magufuli ametoa siku 15 kwa kamati itakayoundwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kukamilisha uchunguzi wa matumizi ya Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Kata ya Mkata, Jimbo la Handeni Vijijini wilayani Handeni.
Utekelezaji wa hatua hiyo utawezesha serikali kupata thamani halisi ya fedha na kuwabaini waliohusika kuhujumu ujenzi huo, ulioshindwa kuendelezwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Alikuwa akijibu kero nne za wananchi wa Mkata zilizotolewa na Mbunge wa Handeni Vijijini, Mboni Mhita pamoja na Diwani wa Kata ya Mkata, Mussa Mwanyumbu, baada ya kuwasili na kudai kusita kwa ujenzi huo kumetokana na serikali kuacha kupeleka fedha kwa miaka miwili sasa na kusababisha usumbufu wa upatikanaji wa huduma ya uhakika kwa wananchi katika kata za Sindeni, Mkalamo, Kang’ata na Mkata pamoja na wasafiri wanaotumia Barabara kuu ya Segera - Chalinze.
“Kero yetu nyingine ni kiwanda cha Mkata Saw Mills kilichotelekezwa baada ya kutaifishwa na serikali mwaka 1998 na kukabidhiwa mwekezaji ambaye mpaka sasa bado hajakiendeleza tunaombwa serikali ikirejeshe kwetu ili wananchi tuendeleze uzalishaji na nyumba nane zilizopo kiwandani wapewe watumishi wa halmashauri yetu ili watekeleze shughuli zao wakiwa hapa hapa Mkata,” alisema.
Awali kabla ya kutoa maagizo hayo, Rais Magufuli alimkaribisha waziri Ummy kujibu kero kuhusu ujenzi wa hospitali, ambao alikiri kuwepo kwa viashiria vya ubadhirifu na kusema kwamba serikali inatarajia kupeleka Sh milioni 800 kuendeleza ili ujenzi. “Ni kweli mheshimiwa Rais, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa sasa haina hospitali, lakini tayari wizara yangu kwa kushirikiana na Tamisemi katika bajeti ya mwaka huu 2017/2018 tumetenga shilingi milioni mia nane kuendeleza ujenzi, lakini tunahitaji kufanya tathmini kwa sababu kazi ya shilingi milioni mia tano zilizotolewa awali ina mashaka ... tumekubaliana kwamba fedha hizo shilingi milioni mia nane hazitakuja mpaka kamati itakapokamilisha kazi,” alisema Ummy.
JKT wapokonywa ardhi Dk Magufuli alisema, “natoa siku kumi na tano kwa hiyo kamati ya kuchunguza ujenzi wa hospitali kukamilisha kazi hiyo kwa sababu tayari yameonekana mashaka hivyo lazima tuyamalize na wale waliohusika kutafuna fedha mimi ndiyo mtumbua majipu na ninawaahidi hilo ili serikali iweze kuleta haraka zile shilingi milioni mia nane kuendeleza ujenzi.”
Aidha, kuhusu kero ya maji, Dk Magufuli alisema serikali imetoa Sh bilioni mbili kutekeleza mradi huo hivi sasa kati ya Sh bilioni nne zinazohitajika kukamilisha mradi wote. Pia alimwagiza Mkuu wa Kikosi cha JKT Kabuku, Luteni Kanal Erasmus Bwegoge kurejesha kwa uongozi wa kijiji cha Kabuku eneo la ekari 50 walizokabidhiwa miaka saba kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata matunda na kumtaka Mbunge wa Handeni Vijijini, Mboni Mhita kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.
Muheza kutiririka maji Akiwa Muheza na Mkanyageni, Dk Magufuli alieleza kuwa serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali mikubwa ya majisafi ili kumaliza kero inayowakabili wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza. Fedha hizo zinajumuisha Sh bilioni mbili kupitia bajeti ya serikali ya mwaka huu pamoja na nyingine Sh bilioni 30 kutoka Serikali ya India ambao utahusisha mikoa 17 nchini, ikiwemo wa Tanga ambao utawakilishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
Aliposimamisha msafara wake mjini Muheza, Rais Magufuli alisema anatambua kero kubwa ya uhaba wa majisafi inayowakabili wananchi hapo na kuahidi kwamba hatawaangusha bali atahakikisha miradi mikubwa ya maji inaelekezea wilayani humo ili kuwezesha wananchi kufurahia maisha. “Ndugu zangu wa Muheza nimesimama hapa na msafara wangu ili niwashukuru sana kwa kunipa kura nyingi za urais na mbunge.
Napenda niwaeleze kwamba kero yenu ya maji naijua na nimeshaanza kuishughulikia kwa kutoka shilingi bilioni mbili katika bajeti ya mwaka huu, lakini fedha hiyo ni sawa na breakfast (kifungua kinywa) tu kwenu mradi mwingine mkubwa wa maji unakuja kutekelezwa hapa,” alisema Dk Magufuli na kuongeza: “Pia nimetenga shilingi bilioni thelathini nyingine kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji hapa kupitia ufadhili wa Serikali ya India.
Fedha kutoka serikali hiyo za kutekeleza miradi ya maji zitapelekwa katika jumla ya mikoa kumi na saba hapa Tanzania na Muheza nimeishachagua kuwakilisha Tanga, wote mnaelewa kwamba ahadi ni deni kwa hiyo sitaki kuonekana kwamba nimesema uongo, bali niwahakikishia kwamba miradi hii ya maji itatekelezwa.”
Mashamba yarudishwa Kuhusu mashamba makubwa ya mkonge, alieleza, “Tayari nilikwishatoa uamuzi kuhusu hekta 14, 000 za mashamba matano kati ya 72 yaliyopo hapa Tanga ambayo hayaendelezwi nimeyafuta na tayari nimempa mkuu wa mkoa ili waweke utaratibu wa matumizi bora ya ardhi lakini asilimia fulani ya ardhi hiyo nimewaagiza igawanywe bure kwenu ninyi wananchi,” Aidha, alibainisha kwamba eneo litakalosalia katika ardhi hiyo litatumika kwa shughuli za uwekezaji wa viwanda ili kuwezesha kupanua wigo wa wananchi kumiliki uchumi wa viwanda kupitia fursa ya ardhi yenye rutuba iliyopo.
Kuhusu Barabara ya Muheza mpaka Amani yenye urefu wa kilometa 35, alisema serikali imetenga Sh bilioni tatu ili kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Akiwa katika mkutano wa hadhara Mkanyageni, alisema serikali imepeleka mradi mwingine wa majisafi wenye thamani ya Sh bilioni 2.9 kutoka Pongwe mpaka Mkanyageni ili kuwezesha wananchi hapo kupata huduma. Awali Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajabu alimpongeza rais kwa kusaidia kupunguza kero ya maji ikiwemo Sh bilioni tano zilizopelekwa katika bajeti ya mwaka huu ili kukarabati mabomba chakavu.
Source: Muungwana
No comments:
Write comments