Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Olusegun Obasanjo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuonesha mfano bora katika Bara la Afrika katika kusimamia uchumi na kutetea maslai ya nchi katika uwekezaji.
Mhe. Rais Mstaafu Obasanjo ametoa pongezi hizo leo tarehe 20 Juni, 2017 muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Mstaafu Obasanjo amesifu juhudi za Mhe. Rais Magufuli kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali duniani na kusimamia ipasavyo sera ya kuhakikisha nchi inanufaika, badala ya kuacha wawekezaji wakijinufaisha wenyewe na nchi kuambulia kiasi kidogo cha mapato.
“Nimepita katika nchi kadhaa zikiwemo Msumbiji, Malawi na sasa nipo hapa Tanzania, na huko kote nazungumzia masuala ya uchumi na namna nchi zetu za Afrika zinapaswa kunufaika na uwekezaji katika maeneo mbalimbali.
“Uchumi wa Tanzania unakwenda vizuri sana, na juhudi za Mhe. Rais Magufuli za kuhakikisha nchi yake inanufaika na uwekezaji ni suala muhimu sana na la mfano, ameonesha mfano mzuri kwa viongozi wa Afrika na hii ndio njia pekee itakayotuwezesha kukuza uchumi wetu, hatuwezi kuendelea kuwaacha wawekezaji wananufaika wao na sisi kuambulia kiasi kidogo sana” amesema Mhe. Rais Mstaafu Obasanjo.
No comments:
Write comments