Wakazi wa kijiji cha Lengijave kata ya Olkokola halmashauri ya Arusha Wilayani Arumeru wamekiri kuwa gharama wanazotumia kutafuta maji ni kubwa kuliko gharama halisi za kulipia maji zinazotozwa na Mamlaka za Maji zilizopo Kisheria.
Wamesema kuwa kijiji chao hakina utaratibu wa kulipia gharama za maji bali huchangishana pale inapotokea changamoto ya uharibifu wa miundombinu ya maji jambo ambalo huwalazimu kutumia muda mrefu na nguvu nyingi ili kupata kiasi kidogo cha maji na kisichotosheleza.
Wameendelea kufafanua kuwa wako tayari kulipia gharama za maji kwa utaratibu utakaowekwa kutokana na adha kubwa ya upatikanaji wa maji wanayoipata wananchi hao licha ya kuwa maji hayo huchotwa bure.
Wameongeza kuwa mradi wa maji wanaotumia ulitengenezwa tangu enzi za mababu zao na mradi huo hauongezeki ingawa idadi ya watu inaongezeka siku hadi siku na kusababisha kiasi cha maji kuwa kidogo pamoja na ubovu wa miundo mbinu iliyotengenezwa miaka mingi iliyopita.
Hayo wameyasema kwenye mkutano kijiji chao baada ya timu ya wataalamu wasimamizi wa mradi wa maji wa 'VIJIJINI VITANO' kutoa mrejesho wa namna maji yatakavyopatikana na jinsi mradi huo utakavyoendeshwa ikiwemo kulipia gharama za maji.
Neserian Lialo mwanamke mkazi wa Lengijave na mfanyabishara amesema kuwa wanawake wa Lengijave hutumia muda wa hadi saa 12 kupata maji licha ya kuwa maji hayo ni ya bure.
Ameongeza kuwa ni kwaida mwanamke kwenda kwenye maji kuanzia asubuhi saa kumi na mbili na kurudi jioni saa kumi na mbili na ndoo mbili za maji akiwa amechoka na shughuli nyingine za nyumbani zikimsubiri.
"Unaamka saa kumi na mbili unaenda bombani unasubiri foleni wakati mwingine ikikaribia kufika zamu yako maji yanakatika unahamia kituo kingine napo unakaa tena foleni na kuambulia labda ndoo mbili za maji" amesema Neseriani
Neserian amesisitiza kuwa wananchi wa Lengijave wako tayari kulipia maji ili muda na nguvu zinazotumia kuhangaikia maji kutumia kufanya shughuli nyingine za kuingiza kipato ambazo wanaamini zitawapatia pesa za kulipia gharama za maji.
"Mimi nafanyabiashara lakini hunilazimu kutenga siku moja nzima ya kuchota maji jambo ambalo limanipotezea muda, naamini nikienda kwenye biashara nitapata pesa zaidi yakuniwezesha kulipia gharama za maji" amesema
Marko Ngaraviti amesema kuwa licha ya kuwa mradi huu wa maji utakuwa ni wa kulipia gharama za maji lakini utakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa Lengijave kutokana na hali halisi ya shida ya upatikana wa maji.
Ngaraviti ameongeza kuwa kulipia gharama za maji litakuwa jambo jema endapo upatikanaji wa maji utakuwa wa uhakika na kuongeza kuwa utaratibu huu tunaushuhudia kwa wananchi wenzetu waishio mijini.
"Sisi tatizo letu hatuna uzoefu wa kulipia maji kwa mfumo ulio rasmi lakini kiuhalisia tunatumia muda, nguvu nyingi pamoja na kuchangishana fedha ili kupata kiasi hiki kidogo cha maji tunachonyang'anyana na wala hakitutoshi" amefafanua Ngaraviti
Mratibu wa Mradi wa maji wa Vijiji Vitano halmashauri ya Arusha Eline Mwanri amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuelewa Sera ya Serikali ya kulipia maji ni kuifanya miradi ya maji kuweza kujiendesha pamoja na usimamizi thabiti wa fedha.
Mwanri ameongeza kuwa mradi umesanifiwa kutumia teknolojia mpya ya kulipia maji kupitia mtandao wa 'eWaterpay' kulipia kabla ya kutumia na zaidi kulingana na matumizi.
" Wananchi wengi walikuwa wanatumia maji bila kulipia, tunakaa na wananchi kuelimishana ili kuwa na uelewa wa pamoja juu ya ulipiaji maji kutumia teknolojia mpya ya eWaterpay" amesema Mwanri
Hata hivyo Mwanri amesema kuwa mradi huo unatekelezwa na shirika la kimataifa la WaterAid kwa ufadhili wa Idara ya Maendeleo ya nchini Uingereza kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 na kutekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wa fedha 2017/2018.
PICHA ZA MATUKIO YA KIKAO CHA WANANCHI KIJIJI CHA LENGIJAVE.
No comments:
Write comments