Na Sulbasia EVord
Wauguzi halmashauri ya Wilaya ya Arusha wilayani Arumeru wametakiwa kuacha tabia ya kufanyakazi kwa mazoea na badala yake kufanya kazi wa weledi na zaidi kwa kuzingatia maadili ya fani ya Uuguzi na yale ya Utumishi wa Umma.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri hiyo Dkt.Wilson Mahera wakati akifungua kikao kazi cha siku moja kilichokutanisha karibu Wauguzi wote wa halmashauri hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Halmashauri ya Arusha.
Dkt. Mahera amesema kuwa fani ya Uuguzi ni nyeti sana inayohitaji umakini, uadilifu, huruma na upendo kwa wagonjwa anaohitaji huduma wakati wakiwa katika hali isiyo ya kawaida.
Ameongeza kuwa Serikali imewaamini Wauguzi na kuwapa dhamana ya kuhudumia wananchi ambao ni wagonjwa na kuwataka kutumia taaluma zao kuhudumia wagonjwa bila kujali hali zao za kiafya wala kiuchumi ili kujenga imani kwa wagonjwa wanaohudumiwa.
Aidha amewataka Wauguzi hao kufanyakazi kwa kushirikiana wao kwa wao kama timu na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma wanazohitaji kwa wakati na kuondoa dhana mbaya iliyojengeka kwa wananchi dhidi ya Wauguzi wa Afya.
"Hakikisheni mnafanyakazi kwa mshikamano katika vituo vyenu vya Afya na kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma anayohitaji kwa wakati hali itakayorudisha uaminifu kwa wagonjwa mnaowahudumia dhidi ya Wauguzi" amesema Dkt. Mahera
Dkt. Mahera ameongeza kuwa fani ya Uuguzi inalalamikiwa sana na wananchi hasa wa hali ya chini kunyanyaswa na kutolewa lugha chafu na baadhi ya Wauguzi punde wanapofika kutibiwa kwenye vituo vya Afya vya Serikali wakati umefika sasa kwa Wauguzi kubadili tabia na kuwahudumia wagonjwa kwa upendo zaidi.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Arusha Dkt.Lucas Kazigo amewataka wauguzi hao kuongeza bidii katika kazi ili kuboresha utoaji wa uduma kwa wagonjwa wote ndani ya halmashauri.
Wagonjwa wanahitaji faraja kutoka kwa Wauguzi jambo ambalo linamtaka Muuguzi kutumia lugha nzuri muda wote kwa wagonjwa.
Ameendelea kusema kuwa Muuguzi anapaswa kutambua kuwa kazi anayofanya ni ya huduma na ni ya kujitoa zaidi bila kulinganisha maslahi.
" Muuguzi anayejitambua afahamu umuhimu wa kazi yake kwa jamii hasa wagonjwa na anatakiwa kujitoa kufanyakazi pasipo kusukumwa wala kulazimishwa" amesema Daktari huyo.
Hata hivyo Kaimu Muuguzi Mkuu Mkoa wa Arusha Getrude Anderson amekemea tabia mbaya ya baadhi ya Wauguzi ya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa kwani ni kinyume cha maadili na pia ni kuidhalilisha fani nzima ya Uuguzi.
" Tuhakikishe tunaacha tabia ya kupokea rushwa kwa wagonjwa sio maadili ya kazi na zaidi ni kujizalilisha kwa wagonjwa na kuidhalilisha taaluma ya Uuguzi, inasikitisha kuomba rushwa kwa mgonjwa ambaye tayari ana tatizo la kiafya " amesema.
Naye Kaimu Muuguzi Halmashauri ya Arusha Agusta Komba amesema kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kuwajengea uweo Wauguzi katika suala la huduma kwa wateja na ukarimu kwa wagonjwa pamoja na uwekaji sawa wa kumbukumbu sahihi za wagonjwa sambamba na huduma wanayoitoa.
" Hapa tunakumbushana tuu maadili ya Uuguzi pamoja na majukumu ya kila siku ya Wauguzi na lengo kubwa ni kuboresha utoaji huduma za Afya kwa wagonjwa kwenye vituo vyote vya Afya halmashauri ya Arusha" amemalizia Komba
PICHA ZA MATUKIO YA KIKAO KAZI HICHO.
No comments:
Write comments