Wednesday, August 16, 2017

Mbunge wa Japan aguswa na folleni jijini Dar es Salaam


Rais Magufuli akiwa na Waziri mstaafu wa Mambo ya Ndani Japan Ichiro Aisawa

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Ichiro Aisawa ameguswa na changamoto ya foleni inayowakumba wakazi wa jiji la Dar es salaam aliyoishuhudia mwenyewe wakati akiwa jijini hapo.

 Aisawa amesema kuwa nchi yake inahitajika kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha miundombinu ya Dar es Salaam kutokana na adha ya foleni kubwa ya magari inayowakabili wakazi wa jiji la Dar es salaam hasa nyakati za asubuhi na jioni.

Aisawa ambaye kwa sasa ni Mbunge nchini Japan amesema hayo  alipokutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo ambapo ameahidi kuyafikisha yale aliyoshuhudia kwa Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe.

Mbali na ahadi hiyo aliyoitoa kuhusu changamoto ya foleni, Mbunge huyo pia amempongeza rais Magufuli kwa jitihada mbalimbali anazochukua katika kukabiliana na rushwa na msukumo mkubwa anaoutoa katika suala zima la maendeleo.

Kwa upande wake Rais Magufuli, amemshukuru Waziri huyo wa zamani kwa kuja Tanzania na kusema kuwa serikali yake inatambua mchango mkubwa ambao Japan imekuwa ikiutoa katika suala zima la maendeleo na itaendelea kukuza uhusiano wake na nchi hiyo.

Pamoja na hayo mgeni huyo wa Rais Magufuli, alitembelea baadhi ya miradi inayoendelea kujengwa hapa nchini na kampuni za Japani, ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara za juu (flyover) wa TAZARA na mradi wa umeme wa Kinyerezi.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo