Jeshi la Polisi limepiga marufuku waendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda kupakia watoto wenye umri chini ya miaka 10.
Jeshi hilo limetoa tamko hilo leo August 15, 2017 na kusisitiza kwamba yeyote atakayekiuka au kukaidi agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na faini, kifungo au vyote viwili
Kamishna Msaidizi wa Polisi ambaye pia ni Afisa Mnadhimu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Theopista Malya, amesema kuwa watoto wamekuwa kwenye hatari kubwa wakipandishwa kwenye Bodaboda na wakati mwingine waendesha bodaboda hubeba watoto zaidi ya mmoja jambo ambalo ni lazima likemewe.
Jeshi hilo pia limewataka wazazi kuacha mara moja kuwapakia watoto kwenye bodaboda na endapo watajulikana kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria kama ilivyo kwa waendesha Bodaboda hizo.
Aidha Kamanda Malya amesema kuwa Jeshi hilo limeandaa kipindi maalumu cha Radio kitakachorushwa na Clouds FM kila siku ya Jumatano saa 2:00 Usiku kikiwa na lengo la kuongeza elimu kwa waendesha Bodaboda katika kuzingatia sheria za Usalama Barabarani pindi wanapofanya shughuli zao.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama barabarani (TSA), John Seka alisema kipindi hicho kitalenga kuwapa elimu waendeshaji wa bodaboda.
Pia, alitumia nafasi hiyo kuwataka wafuate sheria zilizowekwa na Sumatra ili waepukane na mkono wa sheria.
Paulina Shayo ambaye ni mwakilishi kutoka WAT Saccos alisema kuwa wanatoa mikopo kwa bodaboda na kwamba mikopo hiyo itawasaidia kuwa wamiliki halali wa vyombo hivyo.
No comments:
Write comments