Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Mashaka Gambo amepokea msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni thelathini kutoka benki ya NMB Kanda ya Kaskazini kwenye hafla fupi iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari Sokon II Halmashauri ya Arusha.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo Gambo amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa wa Arusha kufanya maandalizi ya kutosha ya kuwapokea wanafuzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwanzoni mwa mwaka ujao 2018 kwa kuandaa miundo mbinu ya madarasa na madawati.
Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa anatambua mchango wa benki ya NMB katika maendeleo ya elimu mkoani Arusha na kuwasisitiza wakurugenzi wote wa halmashauri za mkoa wa Arusha kutumia misaada hiyo kwa maendeleo ya elimu kwenye mkoa huo.
Amesema kuwa vifaa vilivyotolewa na benki ya NMB vitumike kwa matumizi sahihi yaliyokusudiwa na si vinginevyo na kushauri kuvielekeza kwenye maandalizi ya kuwapokea wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018.
Hata hivyo amewataka Wakuu wa shule na Bodi za shule kusimamia vizuri matumizi ya vifaa hivyo ili isifanyike hujuma na msaada kubadilika kuwa mgogoro na si baraka kama ilivyokusudiwa.
" Simamieni matumizi ya vifaa hivi, isije ikatokea msaada huu ukawa chanzo cha kujinufaisha na kuanzisha migogoro baina yenu na kuondoa maana halisi ya baraka hii iliyopatikana" amesema.
Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini Salie Mlay amesema kuwa benki ya NMB ni mdau katika kuchangia huduma za jamii na hutumia asilimia 1% ya faida inayopatikana kila mwaka kurudisha kwenye jamii.
Ameongeza kuwa benki ya NMB inatumia kiasi hicho cha faida kwa kushirikiana na Serikali kupambana na maadui watatu ujinga, masikini na maradhi hivyo hujikita zaidi kuchangia kwenye sekta ya Elimu, Afya na Umasikini kwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali kwa kwa lengo la kupambana na umasikini na kuinua uchumi.
Mlay amevitaja vifaa vilivyotolewa na benki hiyo pamoja na vifurushi 24 vya mabati, mbao 1200 na vipande 300 vya Gipsamu kwa ajili ya kukarabati ofisi za walimu.
Hata hivyo vifaa hivyo vimetolewa kwenye jumla ya shule sita za Sekondari halmashauri ya Arusha ikiwa ni pamoja na shule ya Sekondari Sokon II, Ilkiding'a, Sambasha, Endeves, Olokii na Oldonyosambu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera licha ya kuushukuru uongozi wa benki ya NMB amesema kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa halmashauri iko kwenye mchakato wa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwanzoni mwa mwaka ujao 2018 na kumuahidi Mkuu wa mkoa kusimamia matumizi halisi ya vifaa hivyo.
Amefafanua kuwa vifaa hivyo vitatumika kumalizia vyumba vya madarasa katika shule hizo vyumba abavyo vitatumika kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuongeza kuwa kutokana na ongezeko la wanafunzi halmashauri bado kuna upungufu wa vyumba vya madarasa 41 kwenye shule za sekondari hivyo msaada huo utasaidia kupunguza tatizo hilo.
PICHA ZA MATUKIO YA KUKABIDHI VIFAA VYA UJENZI SEKONDARI YA SOKON II
No comments:
Write comments