Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mh. Josephat Kandege amefanya ziara ya kutembelea na kukagua kituo cha Afya cha Nduruma kata ya Nduruma halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru na kujionea shughuli za utoaji huduma za afya katika kituo hicho.
Pamoja kukagua huduma zinazotolewa kituoni hapo Naibu Waziri huyo amekagua pia eneo litakalotumika kujenga majengo mbalimbali ikiwemo jengo la maabara, chumba cha upasuaji, jengo la mama na mtoto, chumba cha kuhifadhia maiti, nyumba za watumishi pamoja na sehemu ya kuchomea taka, mradi ambao serikali imeshatoa fedha za kuutekeleza.
Naibu Waziri Kadege amesema kuwa serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuendeleza majengo ya kituo hicho cha afya ili kiweze kuwa na hadhi ya Kituo cha Afya kulingana na matakwa ya serikali kupitia Wizara ya Afya.
Aidha Naibu Waziri amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha kuhakikisha kuwa ujenzi wa majengo hayo unakamilika katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa ili wananchi wapate huduma zote kwenye kituo hicho cha Afya.
"Majengo hayo yaanze kujengwa mara moja ndani ya miezi mitatu yawe yamekamilika, hatuhitaji tena mgonjwa afike hapa akose huduma, mgonjwa akifika kituoni apate huduma zote ili asiache kituo hapa na kwenda kutafuta huduma Mount Meru hospital" amesema Naibu Waziri
Amefafanua kuwa lengo la serikali ni kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za wilaya kwa kuhakikisha mgonjwa anapata huduma zote ndani ya kata yake badala yake hospitali za wilaya ziwe ni hospitali za rufaa tuu.
Hata hivyo Naibu Waziri amewataka wahudumu wa afya kituoni hapo kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake kufanya kazi kwa bidii kwa kuweka mbele uzalendo na kuamini kuwa kazi ya uuguzi ni wito inahitaji huruma na upendo bila kuweka mbele maslahi licha ya changamoto ya uchache wa watumishi wa idara ya afya.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha Dk. Wilson Mahera amekiri kupokea fedha hizo na tayari wameshapokea maelekezo ya fedha hizo na zaidi mchakato wa ujenzi umeanza na kuongeza kuwa ndani ya wiki mbili ujenzi utakuwa umeanza.
Dkt. Mahera amefafanua kuwa halmashauri imejipanga kutekeleza mradi huo kwa wakati kutokana na uhitaji mkubwa wa majengo hayo katika kituo hicho cha Afya kwa kuwa eneo hilo liko mbali na hospital ya wilaya ya Olturumet na kuahidi kuhakikisha ujenzi kukamilika ndani ya miezi mitatu kama Naibu Waziri alivyoagiza.
"Natamani ujenzi huu ukamilike hata ndani ya miezi miwili kwa kuwa kituo hiki cha Afya kinahudumia wananchi wa kata tatu Mlangarini, Nduruma hadi Bwawani ambao wako mbali na hospitali yetu ya wilaya ya Olturumeti, huduma ikikamilika hapa itakuwa ni faraja kwa wananchi wetu" amesema Dkt. Mahera
Diwani wa kata ya Nduruma Mh. Raymond Mollel amesema kuwa wananchi wa Nduruma wamepokea kwa furaha neema hiyo na wamekubaliana kuongeza nguvu zao kwa kuchangia kiasi cha milioni 80 kwa kuchangishana kiasi cha shilingi elfu 10,000 kila familia ili kujenga uzio wa Kituo chao cha Afya kwa ajili ya usalama.
"Kituo hiki ni chetu tunaamini ujenzi ukikamilika itaturahisishia kupata huduma kwa kuwa kwa sasa bado kuna changamoto ya kutokupatikana baadhi ya huduma na kufanya watu kuona bora kutumia gharama kwenda kutafuta huduma hospitali za mjini"amesema Diwani
PICHA ZA MATUKIO YA ZIARA HIYO
No comments:
Write comments