Tuesday, August 29, 2017

Serikali yapanga kuokoa Mito iliyo kwenye hatari ya kutoweka Morogoro


Serikali ya Tanzania inaandaa mpango mkakati wa kulinusuru Pori Tengefu la Bonde la Kilombero na kuokoa Mito zaidi ya 140 iliyo katika hatari ya kutoweka kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu katika Pori hilo lililopo mkoani Morogoro.

Afisa wanyamapori mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii Bwana Pelage Kauzeni amesema mpago huo mkakati ukikamilika utasaidia kunusuru uchumi wa nchi na kuokoa wanyama adimu aina ya sheshe ambao kidunia robo tatu ya wanyama hao wanapatikana katika pori hilo.

Amesema vipaumbele vya mpango huo mkakati na shirikishi wa usimamizi wa bonde hilo ni pamoja na kuainisha mipaka ya vijiji na kupanga matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji hatua itakayosaidia kuepusha uharibifu zaidi wa mazingira lakini pia kurejesha wanyama na shughuli za uwindaji wa kitalii katika eneo hilo.

Eneo kubwa la pori tengefu la bonde la kilombero lenye ukubwa wa hekta za mraba zaidi ya 6,000 lipo katika wilaya ya malinyi ambapo akizungumzia hatua hiyo,Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Bwana Marceline Ndimbwa amesema uwajibikaji wa pamoja katika utekelezaji wa mpango mkakati huo ukizingatiwa utawezesha kunusuru rasilimali zilizopo katika pori hilo bonde la Kilombero.

No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo