
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha Dk. Wilson Mahera ametumia muda wake kuwafundisha wanafunzi wa kidato cha II shule ya Sekondari Oldonyosambu somo la Kemia.
Dk. Mahera amefanya marudio kwenye mada ya 'Elements' baada ya kutembelea shuleni hapo kwa shughuli zake za kikazi na kuwakuta wanafunzi wakiwa kwenye maandalizi ya mtihani wa uzamilifu utakaoanza Jumatatu ijayo tarehe 21.08.2017.
Awali mkurugenzi huyo alianza kuwauliza maswali ya somo la Kemia baada ya wanafunzi kujibu maswali hayo kwa kusuasua alijikuta akianza kuwafundisha mada hiyo maarufu kama 'First 20 elements' ambayo ni mada ya msingi kwa wanafunzi wa kidato cha pili.
Mkurugenzi Mahera amasisitiza kuwa mada hii ni msingi wa somo la Kemia hivyo ni muhimu sana wanafunzi kuielewa vizuri bila kukariri jambo litamwezesha mwanafunzi kupata alama kumi kwenye mtihani wa Kemia.
"Mwanafunzi akizielewa vizuri hizi first twenty elements na akajua kuzipanga na kufahamu non metal zinagain electrons na metal zinaloose electrons hawezi kilikosa hili swali na liko section B lina alama 10%.". Amesema Dk. Mahera
Naye Mwalimu wa taaluma shuleni hapo mwalimu Nyangusi Sangeti amesema kuwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne wanategemea kufanya mtihani wa udhamilifu wa kirafiki utakaoshindanisha shule 11 za ukanda wa Ngaramtoni.
Aidha Sangeti amefafanua kuwa mtihani huo ni maalumu kwa ajili ya kuwapima wanafunzi hao kwa maandalizi ya mitihani yao taifa itakayofanyika kuanzia mwezi Novemba 2018.
Pia mwalimu Sangeti amethibitisha kuwa wanategemea wanafunzi wa shule yao kupata matokeo mazuri kwa kuwa wameandaliwa vizuri na zaidi walimu wamemaliza mada zote na kwa sasa wanafanya marudio ya maswali chini ya usimamizi wa walimu wao.
Mwalimu mkuu msaidizi mwalimu Musa Sadi amesema kuwa licha ya juhudi za walimu na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanafunzi wanafaulu mitihani yao lakini bado kuna changamoto ya wazazi kushiriki katika kuwawezesha watoto wao kusoma vizuri.
Mwalimu Sadi ameeleza kuwa baadhi ya wazazi hawawasimamii watoto wao kikamilifu hasa wanapokuwa nyumbani badala yake huwapa kazi nyingi za nyumbani na kuwafanya kushindwa kufanya marudio ya mambo waliyofundishwa shuleni wawapo nyumbani.
"Mwanafunzi akifundishwa darasani akifunga daftari mpaka aje kulifungua tena akiwa shuleni, lakini tunaendelea kuwaelimisha wazazi kuwasimamia watoto wao kwa kuwafuatilia na kuwahimiza kusoma hata wawapo nyumbani na tunawahimiza wazazi kuwalipia watoto wao wakae hostel ili wapate usimamizi wa karibu wa walimu"amesema mwalimu Sadi
Zaidi mwalimu Sadi amedhihirisha furaha yake juu ya hamasa aliyoitoa Mkurugenzi kwa walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Oldonyosambu iliyoonyesha uzalendo na upendo wa kazi ya ualimu.
"Tunamshukuru Mkurugenzi wetu kwa kukazia maarifa kwa wanafunzi wetu hii inatutia moyo hata sisi waalimu kujituma katika kazi na kuhakikisha wanafunzi wetu wanafaulu mitihani yao haijawahi kutokea tangu nimeanza kazi mkuu kuingia darasani na kushika chaki, kwa kweli imetuimpess" amesisitiza
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa kidato cha pili waliopata fursa ya kufundishwa na mkurugenzi Mahera Catherine David ameahidi kufanya vizuri katika mitihani hiyo na hasa katika somo la Kemia kwa kuwa ameelewa vizuri mada iliyofundishwa na mkurugenzi.
"Tumefurahi sana kufundishwa na mkurugenzi na binafsi nimezielewa vizuri first twenty elements na kufahamu namna ya kutambua metal na non metal na sitasahau tena" amethibitisha Catherine
Hata hivyo Dk. Mahera amewataka walimu kujitoa kwa moyo kuwafundisha wanafunzi na kuhakikisha kile wanachokifundisha wanafunzi wanakielewa na si kuwakaririsha na si kufundisha kwa kutimiza wajibu tuu.
No comments:
Write comments