Sunday, August 27, 2017

Mmea wa Azolla neema mpya kwa wafugaji







































Katika kukabiliana na hali yamaisha, siku hadi siku binadamu ameendelea kubuni na kuibua teknolojia mpya ili kupambana na hali ya maisha na mabadiliko ya tabia nchi na kuongeza uzalishaji kwa lengo la kujipatia kipato zaidi.

Wataalamu wa kilimo wamegundua uwezo mkubwa wa mmea wa Azolla wenye utajiri wa virutubisho kwa ajili ya kulisha mifugo aina zote mmea ambao unawezekana kupatikana kwa kuuotesha katika eneo dogo ambalo kila mfugaji anaweza kumudu kuuzalisha.

Afisa Mifugo Halmshauri ya Arusha Sakina Galle  anazungumzia mmea wa Azolla kuwa ni mmea wa asili kutoka jamii ya  ‘Fern plant’ ambao asili yake ni nchini Australia japo kuwa mmea huu kwa sasa umeenea na kuwa maarufu katika nchi za bara la Asia kama China, India hata Afrika.

Katika bara la Afrika Azolla inapatikana katika aina tisa ambazo kati ya hizo aina mbili za mmea wa Azolla zimeshafanyiwa majaribio ambazo kwa kitaalamu ni Azolla Pinnata na Azolla Ficiculoides na zote zinafaa kwa kulishia mifugo.

Galle ameendelea kueleza kuwa mpaka sasa mmea huu  umeanza kuoteshwa nchini Tanzania na kuthibitisha kuwa mmea wa Azolla umeweza kustawi muda mfupi baada ya kuoteshwa na kuonesha mafanikio ya haraka kwa wafugaji.

Licha ya kuwa mmea wa Azolla kuthibitika kuwa na virutubisho bora kwa mifugo Galle  amevitaja virutubisho kuwa ni pamoja na aina nyingi za vitamini, protini, tindikali ya amino na madini muhimu yanayohitajika kwa wanyama na kufanya mmea huo kuwa bora kwa kulishia wanyama wafugwao.

Aidha Galle amesema kuwa virutubisho vinavyopatikana kwenye mmea wa Azolla unatumika mifugo mbalimbali ikiwemo kuku, ng’ombe, mbuzi, kondoo, sungura, nguruwe na samaki.

Galle pia ameeleza namna ya kuotesha mmea wa Azolla na kusema kuwa  mmea wa Azolla unaoteshwa kwenye maji yaliyosimama kwa maana ya kutengeneza bwawa lenye maji kasha kuweka mchanganyiko wa mbegu za Azolla, dawa maalumu ya kupandia, udongo,  mchanga na mbolea ya samadi.

Kwa mara ya kwanza uvunaji wa Azolla unafanyika siku 15 baada ya kuoteshwa na baadae uvunaji hufanyika kila baada ya siku mbili   mpaka tatu na kuendelea kuvuna kwa muda wote.

Aidha mmea wa Azolla unamsaidia mfugaji kupunguza gharama za chakula kwa asilimia hamsini mpaka mia (50% - 100%) kwa kuchanganya mmea huo na vyakula vingine vya mifugo na wakati mwungine mfugaji anaweza kulisha mmea huo peke yake. 

“Virutubisho vya mmea wa Azolla husaidia kupunguza magonjwa kwa mifugo na kuongeza uzito kwa haraka na kwa wanyama kama kuku husaidia kuongeza utagaji wa mayai” amesema Galle.

Aidha Galle  amewataka wafugaji kujifunza kuzalisha na kutumia mmea wa Azolla kulishia mifugo yao kwani upatikanaji wake na rahisi na wa gharama nafuu.



No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo