Licha ya juhudi za serikali kupambana na ukatili wa dhidi ya watoto, halmashauri ya Arusha bado inakabiliwa na tatizo hilo ikiwemo ndoa za utotoni, mimba za utotoni, watoto kubakwa na kulawitiwa pamoja na watoto kupelekwa kuchunga n'gombe badala ya kwenda shule jambo linalotishia kiwango cha ufaulu.
Hayo yamethibitishwa na Afisa Elimu Msingi halmashauri ya Arusha mwalimu Tumsifu Mushi wakati wa Mkutano Baraza la Madiwani wa kuwasilisha taarifa za kata uliofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Afisa Elimu Tumsifu ameyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa ongezeko la wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza na kufafanua kuwa licha ya kuwa tumeandikisha watoto kwa zaidi ya asilimia 100% lakini bado kumekuwa na changamoto ya watoto wenye umri wa kwenda shule kutokuandikishwa na badala yake watoto hao wanaonekana wakichunga ng'ombe.
Ameeleza kuwa Idara ya Elimu imefanya utafiti mdogo kwa kata ya Mwandeti peke yake na kukutana na zaidi ya watoto 100 wenye umri wa kuandikishwa shule wakichunga ng'ombe muda wa masomo jambo ambalo linadhihirisha watoto hao hawakuandikishwa shule.
"Ukitembea kwenye maeneo ya kata ya Mwandeti unakutana na watoto ambao wana umri wa kuanza shule wanazagaa wakichunga ng'ombe muda ambao wenzao wapo shuleni, kwa hali hii hata kama tumeandikisha zaidi ya asilimia 100 lakini bado kuna kundi kubwa la watoto ambao hawajaandikishwa shule" amesema Mushi.
Hata hivyo Mushi ameongeza kuwa halmashauri pia inakabiliwa na tatizo la ndoa za utotoni ambapo takribani watoto 138 wamechumbiwa wawapo shuleni, watoto 71 wa shule ya msingi Engalaoni kata ya Mwandeti na wengine 67 wa shule ya msingi Laroi kata ya Laroi.
"Nikuhakikishie mheshimiwa mwenyekiti tatizo ni kubwa sana na linaathiri hata kiwango cha ufaulu lakini pia kwa sasa jamii imechukulia advantage kuwa mwanafunzi akipata mimba hataruhusiwa kuendelea na masomo hivyo wanapewa mimba ili iwe rahisi kuwaoa kwa hili tunatakiwa kuchukua hatua za haraka sana" amesisitiza
Ameongeza kuwa ukikaa na watoto waliochumbiwa wanasema kuwa siku ambazo si za shule wazazi wanawaamuru kwenda kuwatembelea wachumba zao na mpaka sasa tuna jumla ya kesi 16 za watoto waliozwa katika umri mdogo.
Diwani wa kata ya Mwandeti mheshimiwa Boniface Tarakwa amekiri kuwa na tatizo hilo katika kata yake na kuongeza kuwa kuna tatizo kwenye vyomba vya sheria hasa katika masuala ya mtoto kwani hata watuhumiwa wakipelekwa mahakamani hakuna hatua zozote.
"Hata vijijini tukihangaika kuwakamata wahusika wa matukio hayo tukiwapeleka kwenye vyombo vya sheria baada ya muda mfupi watuhumiwa wanarudi nyumbani, hatujui kesi imeishia wapi, inatuchanganya kabisa" amesema
Diwani Tarakwa ameongeza kuwa mwaka jana kuna wazazi na wanafunzi walikamatwa kwa kutokuwapeleka watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na kupelekwa polisi hawakujua kesi ilipoishia wakatoka na kuendelea na shughuli zao za maendeleo.
Naye Diwani wa kata ya Oldonyosambu mheshimiwa Raymond Lairumbe amesema kuwa mila na desturi za jamii yetu ya kimaasai zimekuwa zikiathi mwenendo mzima wa mashauri yanayohusu ukatili dhidi ya watoto hivyo mahakama kushindwa kupata ushahidi jambo linalosababisha kesi hizo kushindwa kuendelea.
Hata hivyo Wajumbe wa Baraza la madiwani wamekubaliana kuwa na agenda ya kudumu katika vikao vya vijiji na vitongoji ya kuzungumzia na kupiga vita ukatili kwa watoto pamoja na kusaidia kutoa ushirikiano kusimamia kesi za watoto pindi zinapojitokeza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha Mheshimiwa Noah Lembris amesisitiza kuwa Madiwani mnatakiwa kujitoa kusimamia suala pamoja na kuzungumza kwenye vikao madhara makubwa ya ukatili kwa watoto.
"Viongozi muwe na msimamo kwa kuwa mtu akifanya kosa anakimbilia kwa diwani au kwa wazee wa ukoo na mila kuomba asaidiwe, naomba msiwakubalie acheni sheria ifanye kazi ili kukomesha tabia hizo.
No comments:
Write comments