Saturday, August 26, 2017

Watumishi Idara ya Afya watakiwa kufanyakazi kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Halmashauri ya Arusha.


Kama ilivyo ada Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha Dk. Wison Mahera amekutana na watumishi wa Idara ya Afya kwenye Hospitali ya Wilaya ya Olturumet na kufanya nao mazungumzo juu ya utekelezaji wa majukumu yao  ya kila siku.


Mkurugenzi huyo amewataka kufanyakazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za utumishi wa Umma sambamba na kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka kumi wa Halmashauri ambao msingi wake mkuu ni kuifanya halmashauri  ya Arusha kuwa halmashauri inayoongoza Tanzania kwa kujikita zaidi katika kuwahudumia wananchi kwa kutumia rasilimali chache zilizopo.

 Dk. Mahera pia amewasisitiza watumishi hao kutumia taaluma zao kufanyakazi kwa weledi na kuwahudumia wagonjwa ambao licha ya kuhitaji matibabu lakini pia wanahitaji  kuhurumiwa na kutiwa moyo.


"Mnapaswa kufahamu kuwa watumishi wa Umma mmeajiriwa na wananchi ambao ndio mnawahudumia na wananchi ndio wanatathimini kazi mnayoifanya, watumikieni wagonjwa kwa kutumia lugha nzuri jambo ambalo litaondoa malalamiko ya wagonjwa yanayoelekezwa kwenu ya kutumia lugha chafu pamoja na kutunza siri za wagonjwa " amesema


Aidha Dk. Mahera alipata nafasi ya kusikiliza kero na malamiko yaliyowasilishwa na watumishi hao na kufanikiwa kuyatatua palepale yale yanayowezekana ikiwemo yale yasiyohitaji fedha na kuahidi kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa na vifaa vya kutosha ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha 2017/2018.


Hata hivyo Mkurugenzi huyo amewataka watumishi hao kuachana na malalamiko yasiyo ya msingi hasa ya miaka ya nyuma na kuacha kuwatuhumu viongozi wao pale wanapowalazimisha kufuata taratibu za kazi na kuwakumbusha kuwa kuna wakati kiongozi lazima awe mkali sana pale anapogundua kuna uzembe unaosababisha ukwamishaji wa kazi.


"Ukifanya kazi yako kwa kufuata utaratibu, umewahi kazini umetekeleza majukumu yako, umeandika taarifa sahihi ya kazi ulizozifanya nani atakufuata au kukukaripia? achaneni maneno fanyeni kazi ndio kilichokuleta Arusha DC" amesisitiza


Watumishi hao licha ya mvutano wa muda wa muda mrefu wamempongeza na kumshukuru mkurugenzi Mahera na kuahidi kufanya kazi kama timu pamoja na kuwa wawazi kwa kuwa Mkurugenzi huyo anahitaji uwazi zaidi.

Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya watumishi Afisa Ustawi wa Jamii Mashaka Nkole amesema kuwa tunakupongeza mkurugenzi na uongozi wa halmashauri kwa kuwa kwa kipindi kifupi Idara ya Afya imekuwa na mafanikio makubwa hasa kwa halmashauri kuelekeza nguvu kutatua changamoto kwenye maeneo ya huduma za afya  zahanati , vituo vya afya hadi hospitali.

"Mkurugenzi nikupongeze kwa kuwa umefanya mabadiliko makubwa kwenye sekta ya Afya kwa kuboresha vituo vya afya na hata kukaa na sisi watumishi kusikiliza kero zetu jambo ambalo linatutia hamasa ya kufanyakazi kwa bidii" amesema Nkole


Naye Afisa Utumishi Maimuna Ilonga amewasisitiza watumishi hao kutafuta taarifa zinazohusu masuala mbalimbali  ya utumishi  hasa yanayohusu haki na wajibu wa watumishi kwa kuwa taarifa hizo zinapatikana hata kwenye mitandao kupitia tovuti ya tume ya utumishi wa Umma badala ya kusubiri mpaka afisa utumishi akuletee na kuishia kulalamika.



No comments:
Write comments

Matangazo

Matangazo