Kufuatia dhima ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi kwa kutumia rasilimali zinazopatikana nchini, halmashauri ya Arusha inatekeleza kwa vitendo adhma hii kwa kugharamia mafunzo ya kufyatua matofali pamoja na kuwakabidhi mashine ya kufayatulia matofali kwa vikundi vya vijana.
Halmashauri ya Arusha kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imetoa mafunzo kwa vikundi vya vijana wahitaji kata ya Nduruma na Oljoro ya kufyatua matofali yenye kutumia gharama nafuu kwa kutumia udongo wa asili na kiasi kidogo cha saruji.
Afisa Maendeleo ya Jamii kitengo cha Ufundi ndugu Vitus Chigogolo akizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo kwa vikundi kwenye ofisi kata ya Nduruma amesema kuwa halmashauri inagharamia mafunzo haya yenye lengo la kuwajengea uwezo vijana walio tayari kwenye vikundi kutengeneza matofali yenye kutumia gharama nafuu ambayo yatawawezesha kijana kujipatia kipato.
Chigogolo amefafanua kuwa tunawafundisha kutengeneza matofali yanayofungamana ambayo yanatengenezwa kwa gharama nafuu sana tofauti na matofali mengiene kwa kutumia udongo wa asili na kuchanganywa na kiasi kidogo cha saruji na baada ya mafunzo haya tunawachia mashine ambayo wataendelea kuitumia kama mtaji wa kuanzia kazi.
“Tunategemea baada ya mafunzo haya vijana hawa watakuwa tayari wana mtaji wa kuanza kufyatua matofali kazi yao kubwa ni kutafuta wateja wa kuwauzia matofali hayo” amesema Chigogolo
Kikundi cha vijana Unguuni Youth Group kinachojishughulisha na kilimo wameamua kujiingiza pia kwenye shughuli ya kufyatua matofali mara baada msimu wa kilimo kumaliazika.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Unguuni ndugu Emanuel Tengeneza amesema kuwa tumeamua kupata ujuzi wa kufyatua matofali ili msimu usio wa kilimo tutumie muda huo kufyatua matofali kwa ajili ya kujiongezea kipato na kuinua uchumi wetu na familia zenu.
“Huku kwetu tuna msimu mmoja wa wa kilimo wakati usio wa kilimo huwa tunakuwa tunabangaiza bangaiza sasa kwa mafunzo haya tutatumia muda huo kuimarisha mradi wa kufyatua matofali na tunaamini tutapata fedha nyingi kutokana na mradi huu” amesema Tengeneza
Aidha Tengeneza amesema kuwa licha ya kuwa watafyatua matofali kwa ajili ya biashara, kikundi kina ndoto ya kutoa sehemu ya matofali kujenga choo kwenye ofisi ya kata ya Nduruma pindi watakapoanza, lengo ni kuhudumia jamii pamoja na kutangaza biashara.
Afisa Vijana halmashauri ya Arusha Ahadi Mlai amesema kuwa mafunzo hayo wanayatoa kwa vijana wanaoomba kupatiwa mafunzo na baada ya mafunzo hupatiwa mashine moja kwa kikundi ambayo huanza kuitumia kama mtaji kwa uangalizi na usimamizi wa wataalamu wa halmashauri.
“Baada ya mafunzo tukiwaachia mashine tunaendelea kuwasimamia kuangalia mwenendo wa kazi na kutoa ushauri mpaka tuhakikisha wameweza kusimamia wenyewe mradi wao” amesisitiza Mlai.
Hata hivyo Mlay amesema kuwa licha ya juhudi za serikali kuwaelimisha vijana kujiunga kwenye vikundi ili kupata fursa zinazotolewa na serikali lakini bado kuna changamoto kibwa ya vijana kukibali kuunda vikundi na kufanya shughuli ya pamoja jambo ambalo linawakosesha sifa ya kupata mikopo ya vikundi inayotolewa na serikali.
"Sifa moja wapo ya kikundi cha vijana kupata mkopo ni kuwa na shughuli ya pamoja na iliyosajiliwa kama kikundi, hili limekuwa changamoto kwa kundi la vijana kutokana na kutokuaminiana, hofu ya kudhulumiana pamoja na vijana kupuuzia mambo kutokuwa na majukumu" amesema Mlai
Mafunzo hayo pia yametolewa kwa vikundi vingine vya vijana wa kata ya Oljoro ambayo yanategemewa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kitabia kwa vijana ambao wengi wao walikuwa wamekata tamaa kutokana na kukosa ajira.
Monday, August 7, 2017
Vikundi vya viijana Nduruma vyapatiwa mafunzo ya kufyatua matofali
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Write comments